Zitto amejikwaa, hajaanguka

MSIMAMO wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kuhusu suala la ununuzi wa mitambo ya kuzalisha umeme ya Dowans unaonekana kuwakwaza watu wengi.
Wapo ambao wamefikia mahali pa kumuona kuwa mbunge huyu sasa ni fisadi au amepewa “kitu kidogo.”
Wengine wameumizwa na msimamo huo kwa kuona kuwa “mbunge wao” ambaye ameonekana ni mtetezi imekuwaje sasa akawageuka.
Nimepata bahati ya kuzungumza na Zitto mara nyingi na kukutana ana kwa ana. Ninaweza kusema kitu kimoja ninachoamini ndicho kimemponza katika suala hili. Zitto anaamini sana katika kile anachokiita “maslahi ya taifa.” Kuweza kuelewa hili niwakumbushe kwenye suala la Buzwagi.
Baada ya kufungiwa kuhudhuria vikao vya Bunge, Zitto akiwa na viongozi wengine wa upinzani walifanya mikutano mbalimbali iliyovutia maelfu ya watu nchini kote.
Nilimuuliza wakati ule kwa nini hawakutumia nafasi ile kukijenga chama chao kwa kuandikisha wanachama wapya kwani ilikuwa nafasi nzuri ya kisiasa? Jibu lake ambalo nalikumbuka mpaka sasa ni kwamba hakutaka kulivisha siasa suala hilo.
Kwa maneno mengine, hakutaka kufanya suala la Buzwagi kuwa mradi wa kisiasa wa kumpatia yeye na chama chake umaarufu. Kwake suala hilo lilikuwa ni la kitaifa zaidi kuliko la kichama.
Katika mjadala wa Dowans ambao tumeufanya kwenye mtandao wa Jamiiforums.com nilipata tena kuona hisia hizihizi.
Nilivyomuelewa (na sijazungumza naye moja kwa moja tangu suala hili lianze) ni kuwa kununua mitambo hiyo ilikuwa na umaana wa kuepusha matatizo ya sasa ya nishati na kuwa msimamo wake ni wa Kamati ya Bunge anayoiongoza.
Bahati mbaya sijaona mapendekezo ya kamati hiyo. Hata hivyo, ninaelewa kuwa kwa Zitto kutatua tatizo la umeme sasa hata ikibidi kununua mitambo ya Dowans ni kubwa zaidi kuliko wasiwasi wa nani ni mmiliki. Kwake yeye suala ni tuepushe kupungukiwa na umeme halafu hayo mengine tuhangaike nayo baadaye.
Hapa ndipo ninaamini lilipokuwa kosa lake. Kwa vile ameshindwa kuangalia suala hili kwa mwanga wa kisiasa, ndiyo maana amejikuta hajaeleweka kwani sisi wengine tumeona tatizo la kisiasa ambalo hatimaye limesababisha Tanesco kukaa pembeni.
Kisiasa hakukuwa na uwezekano wa aina yoyote ile kuwa kampuni iliyoingia kitapeli (kama nitakavyoonesha siku si nyingi zijazo, inshallah), imeshapewa mabilioni ya fedha zetu, imetushtaki huko Paris, mmiliki wake “hajulikani;” sasa ipewe fedha nyingine kwa mitambo ambayo tayari tumeikataa.
Kama kampuni yenye mitambo hiyo ingekuwa ni nyingine na isiyotajwa kwenye mambo ya kifisadi na siyo katika mazingira kama haya, nina uhakika kungekuwa hakuna pingamizi. Tatizo kubwa la suala hili linahusiana moja kwa moja na kampuni yenyewe ya Dowans.
Hivyo, kutetea ununuzi wa majenereta ni sawa, lakini unapoongeza kuwa tununue toka Dowans hapo inakuwa kimbembe.
Hivyo, Zitto alishindwa kuona mtazamo wa kisiasa, kitu ambacho kinatokana na msimamo wake wa kujali kile anachopenda kuita, “maslahi ya taifa.”
Nadhani kwa kadiri siku zinavyokwenda ndivyo atakavyotambua kuwa siasa ni sehemu kubwa sana ya maamuzi mengi ambayo viongozi wanatakiwa kuyafanya na ataanza kuchukulia gharama ya kisiasa ya maamuzi hayo.
Hata hivyo, kuwa tofauti na watu wengi haina maana yeye naye ni fisadi au kanunuliwa. Kutokana na rekodi yake katika uongozi wa taifa letu ni wazi kuwa hatuna budi kumpa imani na kusema tu kuwa katika hili alipotea.
Tukubali kuwa anajifunza siasa na polepole ataelewa uzito wake. Kama atakuwa amechukua uamuzi huo kwa sababu nyingine yoyote ile nje ya mtazamo tofauti au kuchukua msimamo wa kushawishiwa na nguvu yoyote, basi na yeye atalipa gharama yake.
Ninayaamini maneno yake aliyoyaandika kwenye Jamiiforums.com pale aliposema, “ni vema sana tujifunze kuheshimu maamuzi ya watu wengine. Kwamba leo mtu akiamua usivyotaka kanunuliwa? Je hayo maamuzi mengine hayawezi pia kuwa ya kununuliwa? Hapana, nadhani pale ambapo mwingine ana maamuzi tofauti ni vema kuheshimu maamuzi hayo bila kumwita kila aina ya majina mabaya.”
Zitto kachukua uamuzi ambao siyo wenye sifa zaidi au unaokubalika zaidi; kachukua msimamo ambao kisiasa unaweza kumletea matatizo. Lakini amechukua uamuzi na kausimamia. Yawezekana umemfanya ashukiwe na watu au kuonekana naye ni kuwadi wa mafisadi.
Lakini ukweli ni kwamba hadi hivi sasa kati ya wabunge wetu wengi anasimama peke yake kama ishara ya kuthubutu na uongozi usiotetereka. Anasimama peke yake kama mbunge ambaye alionewa na mamia ya wabunge wenzake na kubezwa na walio kwenye madaraka juu yake. Alisimama peke yake.
Nasema Zitto amekosea kisiasa na katika suala hili hakutakiwa kuwa upande aliopo. Hata hivyo heshima yangu kwake, na imani yangu kuwa tukimpa nafasi ndivyo atakavyoweza pia kujifunza maamuzi ya kisiasa ambayo wakati mwingine yanaweza yasionekana ni maslahi ya taifa vilevile.
Ni katika kukosea ndivyo tunajivunza na ni katika kunolewa ndipo tunakuwa na makali.
Zitto anajua msimamo wangu kwenye Dowans tangu mwanzo; naheshimu msimamo wake kama vile ninavyoheshimi misimamo ya waheshimiwa Mwakyembe, Selelii na wengine. Siku Mwakyembe au Selelii akichukua msimamo tofauti na wa kwangu au wa kuunga mkono kitu ambacho nakipinga haina maana kanunuliwa na mafisadi.
Maana yake ni kwamba ni kiongozi kweli anayethubutu kuchukua msimamo ambao dhamira yake inamtuma. Haogopi kuchukua msimamo ambao unaweza kuwakwaza marafiki zake na kumtenga na ndugu zake. Hao ndio viongozi tunaowataka.
Tumewachoka viongozi wanaofuata mkumbo au ambao wanachukua maamuzi kwa kuogopa kuwaudhi marafiki au wafadhili wao. Tumechoka viongozi ambao kwa sababu ya urafiki wanajifanya ati hawajui Dowans ni nani; kama vile vile wanavyojua Kagoda ni nani!
Ni hao hao ambao wanajifanya ati hawajui Meremeta ni nani kama vile hawajui Mwananchi Gold ilipeleka fedha wapi.
Zitto kakosea lakini pia yuko sahihi. Kakosea kutetea ununuzi. Na Dowans wasifikiri kuwa wana mtetezi, kwani bado Zitto ni mtetezi wa Watanzania. Hapa amejikwaa, hajaanguka.